THE MODERN WAR

(Vita ya kisasa)
Sehemu ya………01
Mtunzi: Saul David

UTANGULIZI
Mwanzo ilikuwa ni vita rahisi sana, vita dhidi ya ndugu yangu wa damu aliyeenda kinyume na kanuni za maisha ya utu. Sikujua kwa kufanya hivi ningeamsha vita nyingine kubwa ambayo ipo juu kabisa ya uwezo wangu na uwezo wa nchi yangu. Vita na ndugu yangu imegeuka na kuwa vita ya ulimwengu mzima.

Cha ajabu ni kwamba ili kushinda vita hii haihitaji mtutu wa bunduki wala siraha yoyote. Natamani kuacha kupambana lakini siwezi kwa sababu tayari nimeshaanza. Kuendelea maana yake nimekubali kuwakabili maadui wenye rangi nyeupe ambao wamejipanga kwa zaidi ya miaka 10 kuhakikisha wanashinda.

Hatima ya Dunia yangu, Nchi yangu, Rais wangu, ndugu na familia yangu ipo mikononi mwangu. Kwa bahati mbaya ni kwamba licha ya nchi yangu kuwa na uwezo mdogo wa kupambana lakini imejikuta inatumika kama chungu cha kuandalia vita hii kali bila kujua, isitoshe tunapigana na kitu tusichokiona.

Naweza kusema sasa ni wakati wa mapenzi, sayansi na teknolojia kuipeleka Dunia vile inavyotaka.
Naam kwa mara ya kwanza historia inakwenda kuandikwa, historia ya vita ambayo haijawahi kutokea popote duniani, ndio sababu nasema hii ni VITA YA KISASA (THE MODERN WAR) niite Inspekta Aron”

SEHEMU YA KWANZA- (KIFO CHA SHAHIDI WA MWISHO)

SASA TUANZE SIMULIZI YETU….

“Mume wangu niue mimi, muache mwanangu aishi tafadhali bado ni binti mdogo naomba usimuue”
“Mama naogopa…!”

“Usiogope mwanangu kila kitu kitakuwa sawa, usijali sawa Annah”
“Mheshimiwa, mtihani ulionipa ni mgumu sana hivi nawezaje kumuua mwanangu au mke wangu, naanzaje kumwaga damu zao”

“Kama huwezi basi acha nitakusaidia mimi mwenyewe, nimekwambia chagua moja umuue mtoto wako au mke wako”

“Mheshimiwa siwezi tafadhali nipe adhabu nyingine, waache mke wangu na mwanangu waondoke nitafanya chochote unachotaka, niko chini ya miguu yako mkuu”

Haya yalikuwa ni mazungumzo ya watu zaidi ya watano waliokuwa ndani ya jengo moja chakavu lililokuwa limetelekezwa kabla ya ujenzi kukamilika, jengo hilo lilikuwa limejitenga pembeni kidogo ya mji.

Alikuwepo Dokta Isaack Gondwe ambaye ni waziri wa afya akiwa na vijana watatu nyuma yake ambao wote walikuwa wameziba nyuso zao kwa vitambaa vyeusi. Walikuwa wamesimama mbele ya familia moja ya watu watatu yaani baba mama na binti yao mdogo mwenye umri wa miaka 22 aliitwa Annah.

“Baba Annah nimekukabidhi bastola umuue mmoja kati ya mke au mtoto wako kisha nikuache uende lakini umeshindwa, basi acha vijana wangu wafanye kazi yao” alisisitiza Dokta Gondwe huku akibinua mabega yake kwa kejeri

Kwa mara nyingi tena Baba Annah aliinua juu mkono wake wa kulia ulioshikilia bastola akaielekeza walipokuwa wamesimama mke na binti yake Annah, hali akitetemeka alivuta pumzi ndevu na kuishusha taratibu, kijasho chembamba kikawa kinamtoka mzee huyo.

Mama Annah alimkumbatia binti yake akamziba usoni na kiganja cha mkono wake hakutaka mwanae aone kinachoendelea, naye akafumba macho kwa uchungu akiwa tayari kwa lolote litakalotokea.

Mara ghafula Baba Annah aligeuka kwa kasi akabadilisha uelekeo na kuilekeza bastola yake walipokuwa wamesimama Mheshimiwa dokta Isaack Gondwe na vijana wake, bila kusita akabinya kitufe cha kufyatua risasi huku akiwa amemlenga Dokta Isaack Gondwe kichwani lakini risasi haikutoka ,akajaribu tena mara ya pili na ya tatu lakini hali ikawa ni ile ile, baba Annah akahisi kuchanganyikiwa.

“Hahahah, ha ha ha, ha ha ha haaa” Dokta Gondwe alicheka tena kwa sauti kubwa sana, kisha akaongea
“Nilijuaa…! nilijua tu wewe ni msaliti, unajifanya mjanja sio? ona sasa umeumbuka mbele ya familia yako mzee hii ni mara ya pili unanisaliti, niliwaomba msitoe ushahidi wowote mahakamani lakini mkapanga kunigeuka wewe na familia yako pamoja na kukuhonga pesa nyingi bado ukapanga kunigeuka. Sasa unanisaliti tena kwa mara ya pili unataka kuniua, bahati mbaya bastola niliyokupa haina risasi hahahaha”

“Ulaaniwe Dokta Gondwe, mungu akulaani, utakufa kifo kibaya, wewe na watu wako wote mtakufaa, hata hicho cheo ulichonacho najua ni cha dhuruma, nakwambia utakufa” Baba Annah aliishia kutoa laana kwa mheshimiwa Dokta Isaack Gondwe mara baada ya kubaini kuwa hana ujanja tena.

“Acha makelele yako, laana kama hizo zilishakuja nyingi sana, hata marehemu mama yangu alinilaani tangu nikiwa tumboni lakini hadi leo hakuna laana iliyofanya kazi” alisema Dkt Gondwe huku akiinamisha kichwa chake chini kutega sikio kumsikiliza kijana wake mwingine ambaye aliingia ndani ya jengo hilo wakati anazungumza.

Kijana huyo hakuwa amefunika sura yake kama wengine, alimnong’oneza maneno kadhaa kwa takribani sekunde 30 hivi, Dokta Gondwe akaonekana kushtuka kiasi kisha akapaza sauti akifoka.

“Kwa nini, kwa nini kila siku yeye tu? hii inawezekanaje? kajuaje tuko hapa? huyu mdogo wako anataka nini? kwa nini unashindwa kumdhibiti? hivi askari ni yeye tu hakuna wengine aah!” Dkt Gondwe alifoka huku akiondoka, akapiga hatua kadhaa kisha akageuka tena.

“Unajua cha kufanya Tino, natangulia kwenye gari” alisema Dkt Gondwe kisha akatoka nje ya lile jengo.
Tino ambaye ndiye aliyeonekana kuwa na mamlaka kuliko vijana wengine wa Dkt Gondwe, alichomoa bastola iliyokuwa kiunoni kwake. Bila kuuliza alimfyatulia risasi Baba Annah, risasi iliyopenya sikio la kushoto ikatokea sikio la kulia, alifanya hivyo pia kwa Mama Annah, kisha akamalizia kumpiga risasi ya kifua Annah. wote wakaanguka chini na kupoteza maisha.

Lilikuwa ni tukio kubwa na zito, kuua watu watatu kwa wakati mmoja. Lakini kwa Tino ilikuwa ni tofauti kabisa, alifanya kwa urahisi sana kama anakunywa maji vile, ilionyesha wazi hii ilikuwa ni kazi aliyoizoea.
Baada ya kufanya hivyo Tino na wale vijana wengine waliandaa mazingira kuonyesha kuwa Baba Annah alimuua mke na mtoto wake kwa kuwapiga risasi kisha na yeye akamalizia kwa kujipiga risasi mwenyewe.

Baadae walitoka na kuingia ndani ya gari mbili zilizoegeshwa nje ya jengo hilo, wakaondoka kwa kasi kuwakimbia polisi ambao kwa mujibu wa maelezo ya Dokta Gondwe alimaanisha wapo njiani wanakuja na mmoja kati ya polisi hao ni mdogo wake na kijana wake wa kazi yaani Tino.
⭐⭐⭐

Ni kweli, dakika chache tu baada ya Dokta Gondwe na vijana wake kuondoka, gari za polisi zisizopungua sita zilifika na kufunga breki kali nje ya jengo hilo na punde polisi walishuka na kuanza kumiminika kwa kasi kuingia ndani ya jengo hilo huku siraha zao zikiwa mbele Ilikuwa ni ishara tosha kuwa polisi hawa walikuwa na taarifa kamili ya kile kilichokuwa kinaendelea ndani ya jengo hilo.

Walikagua vyumba vyote vya jengo hilo, hawakupata mtu yeyote zaidi ya miili ya Baba Annah mama Annah na Annah mwenyewe, kwa haraka haraka ilionyesha wazi kuwa Baba Annah ndiye aliyetekeleza mauwaji hayo kwani mkono wake wa kulia alishika bastola iliyotumika.

Lakini hicho sicho alichokuwa akikiona na kukiwaza Inspekta Aron, kijana ambaye ni polisi mpelelezi kutoka kituo cha kati Handeni. Yeye aliyatazama mazingira ya mle ndani kwa utulivu wa hali ya juu, akaitazama ile miili mmoja baada ya mwingine huku akichukua baadhi ya vielelezo muhimu kama ilivyokuwa ada kwa polisi wengine.

“Tumempoteza shahidi mwingine” Alisema Inspekta Jada, polisi ambaye alikuwa akifanya kazi kwa ukaribu sana na Aron. “Yah! tumechelewa kidogo sana, tungewahi tungeweza kuwaokoa pengine” alisema Aron huku akisogea pembeni pamoja na Jada wakiwaacha polisi wengine wakiendelea na kazi.

“Huenda walipata tena taarifa kama tunakuja” Alisema Jada
“Usiseme huenda, huo ndio ukweli wenyewe Inspekta Jada hii serikali ina watu wa hovyo sana” Aron alilalamika “Usijali Aron jitihada zako zitazaa matunda siku moja, ki ufupi unajituma sana, uwe na subra siku moja tutawakamata wote”

“Inshallah iwe hivyo, lazima nitamkamata Tino”
“Mmh! unahisi kaka yako Tino kahusika kwenye hili tukio pia”
” Ndiyo lazima alikuwepo hapa, subiri uone” Alisema Inspekta Aron akachukua simu yake akaitafuta namba aliyoihifadhi kwa jina la ‘Bro Tino’ akapiga. Simu iliita kwa dakika kadhaa bila kupokelewa mwisho ikakata, akapiga tena.
⭐⭐⭐

Upande wa pili Tino na bosi wake ambaye ni Waziri wa afya Mheshimiwa Dokta Isaack Gondwe tayari walishafika mjini. Tino akiwa ndiye dereva alikuwa ameegesha gari pembeni ya barabara na pembeni ya gari hiyo kulikuwa na gari nyingine ya serikali V8 ilikuwa imepaki ikimsubiri Dokta Gondwe ambaye bado alikuwa na mazungumzo na kijana wake tegemezi Tino.

“Tino, kama sikosei hii ni mara ya nne kama sio ya tano nakwambia kuhusu huyu mdogo wako Inspekta Aron unaemlealea sana, hili ni bomu ambalo litakuja kutulipukia baadae” Dkt Gondwe aliongea kwa msisitizo

“Usijali bosi, huyu ni mdogo wangu najua namna ya kumdhibiti niachie mimi, kuwa na amani bosi” Tino aliongea kwa kujiamini huku akipiga jicho pembeni kuitazama simu yake iliyokuwa ikiita mpigaji akiwa ni Aron mdogo wake.

“Haya mimi nakwenda, tayari tumeshaua mashahidi wote nina hakika tutashinda kesi mahakamani na mkwe wangu Osward atakuwa huru, lakini jua vita yetu bado ni kali sana na ndio kwanza tunaanza”
“Sawa mkuu”

Dkt Isaack Gondwe alishuka kwenye gari akapiga hatua na kuingia kwenye gari nyingine ile V8 dereva akawasha gari wakaondoka. Tino aligeuka na kuitazama simu ambayo ilikuwa ikiita kwa mara ya pili sasa, akapokea.

“Nambie dogo”
“Ulikuwa hapa Tino, ni wewe tena si ndiyo?” Inspekta Aron alisikika upande wa pili akiuliza
“Wapi mbona sikuelewi unazungumzia nini?”

“Najua unanielewa vizuri bro, sasa sikia nakuhakikisha kwamba lazima nitakukamata, nitathibitisha uchafu wako wote, mtafungwa wewe pamoja na mtandao wako mzima”

“Come down mdogo wangu, punguza vitisho huna ushahidi wowote wa kunifunga na hautokuja kufanikiwa kamwe, sahau” “Nisikilize kwa makini kaka labda nisiwe hai, yaani kwa mikono yangu nitakupeleke je…”
“Kaa kimya Aron huna faida yoyote wewe, nahangaika usiku na mchana kutafuta mamilioni ya pesa kwa ajili ya matibabu ya mama yetu, lakini wewe unafanya nini? unahangaika kutaka kunizuia, unaakili kweli wewe?”

“Mama yangu hawezi kuendelea kutibiwa kwa pesa zako chafu kaka, hata angekuwa anajitambua ninauhakika asingekubali hili”

“Kwa hiyo unatakaje, nimuache afe?”
“Kufa au kupona kwa mama yangu ni mpango wa Mungu sio wako Tino”
“Ni mama yetu sio mama yako, kumbuka hilo” alisema tino kisha akakata simu kwa hasira

“Vipi amesemaje?” Aliuliza Inspekta Jada mara tu baada ya kukata simu. “Kauli zake ni zile zile za kila siku, anadai anatafuta hela kwa ajili ya mama kule hospitali” Aron alijibu kinyonge.

“Pole Aron, nakuonea huruama sana, mungu akufanyie wepesi ni miezi sita mpaka sasa unapambana kwa ajili ya matibabu ya mama yako gharama ni kubwa lakini bado kaka yako naye anazidi kukuchanganya” alisema Inspekta Jada akionekana kuguswa na hali aliyokuwa akiipitia Inspekta Aron. Kabla Aron hajazunguza chochote mara kuna askari alionekana akikimbia kuwafuata, akafika na kusimama mbele yao huku akihema kwa nguvu.

“Vipi kwema?” aliuliza Aron akionekana mwenye shauku ya kujua kilichomleta, vivyo hivyo kwa Jada.
“Yu..yule binti kule nda..ndani ha..hajafa ni mzima” alisema yule askari kauli iliyowafanya Aron na Jada watazamane.

Je, nini kitafuata?
Nini hatima ya Vita kati ya ndugu hawa wawili yaani Aron na Tino?
Kwa nini Tino yupo karibu na Waziri wa afya?
Annah hajafa ni mzima huu unaweza kuwa ushahidi wa mwisho wa Inspekta Aron?
Kwa nini VITA YA KISASA?

Hii ni sehemu ya kwanza, majibu ya maswali haya utayapata ndani ya simulizi hii maridhawa iliyojaa visa vingi vya kusisimua. Mauaji, tamaa, mapenzi, urafiki, hila,chuki, drama, vita, usaliti, siasa, visasi, mahaba, kushinda na kushindwa pamoja na mambo mengine yasiyotazamiwa bila kusahau LOVE STORY kali ndani yake.

Naam hii ndio MODERN WAR(vita ya kisasa)

THE MODERN WAR
(vita ya kisasa)
Sehemu ya……….02
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047.

02-( KIKAO CHA SIRI)
ILIPOISHIA 01…
“Vipi kwema” aliuliza Aron akionekana mwenye shauku ya kujua kilichomleta, vivyo hivyo kwa Jada.
“Yu..yule binti kule nda..ndani , ha..hajafa ni mzima” alisema yule askari kauli iliyowafanya Aron na Jada watazamane

SASA ENDELEA….
“Nini? Unauhakika?” Aliuliza Aron
“Ndiyo afande, yule binti ni mzima hajafa”
Haraka Jada na Aron walikimbia kuelekea ndani ya lile jengo kwenda kuhakikisha ukweli wa taarifa hiyo
“Jada ita gari ya wagonjwa upesi” Alisema Aron huku akiendelea kukimbia lakini mara akasimama na kumtazama Jada ambaye tayari alishatoa simu mfukoni.

“Hapana usipige, mwite Dokta Zyunga afike hapa haraka na vifaa vyote muhimu tutampeleka hospitali kwa siri hatakiwi kujua mtu mwingine zaidi yetu” alisema Inspekta Aron, Jada akafanya kama alivyoagizwa.

Nusu saa baadae Inspekta Aron mdogo wake Tino alikuwa ndani ya hospitali kubwa ya kimataifa maarufu kama MOUNTENIA HOSPITAL, Aron alikuwa amesimama nyuma ya mlango mkubwa wa kioo uliokuwa na maandishi makubwa juu yake yaliyosomeka ‘MAJOR THEATER'(Chumba cha upasuaji mkubwa). Aliwatazama madaktari waliokuwa wakiendelea kupambana kuyaokowa maisha ya Annah ambaye alifikishwa hospitalini hapo kwa siri kubwa. Tayari Annah alikuwa ameshawapoteza wazazi wake wote wawili waliouwawa kikatili masaa machache yaliyopita ikiwa ni agizo la Waziri wa afya Dokta Gondwe.
Madaktari walifanikiwa kuitoa risasi iliyokuwa imezama upande wa kulia wa kifua cha Annah. Kwa bahati nzuri risasi haikuwa imeleta madhara wala kugusa viungo muhimu kama mapafu na ini, kwa sasa jitihada nyingine za kibingwa zilikuwa zikiendelea kuyanusuru maisha ya binti huyo yatima.
Inspekta Aron aliendelea kusimama pale nje huku akimuomba mungu wake ayaokoe maisha ya binti huyu muhimu sana kwake.
“You’re my last hope Annah, please don’t die”(wewe ndio tumaini langu la mwisho Annah tafadhali usife) Alisema Inspekta Aron huku akiwa amekutanisha mikono yake kumuomba mungu
Annah alikuwa ndiye shahidi pekee aliyehai dhidi ya kesi ngumu ya mauaji aliyofanya kijana Osward ambaye ni mkwe wa Dokta Gondwe. Kesi hiyo ilikuwa ni daraja pia la kuwatia hatiani kaka yake Tino pamoja na Waziri wa afya Dokta Gondwe ambao wamekuwa wakifanya matukio mengi ya kiharifu lakini anashindwa kuwatia nguvuni kwa sababu ya kukosa ushahidi.

Upande wa pili ndani ya hoteli moja kubwa ya kifahari Waziri wa afya Mheshimiwa dkt Isaack Gondwe alionekana akiwa katika kikao cha siri yeye pamoja wa wazungu watatu, alikuwepo pia Rais mstaafu wa awamu ya nne mheshimiwa Profesa Cosmas Kulolwa pamoja na mkemia mkuu wa serikali bwana Andiwelo Katabi. Kilikuwa ni kikao cha siri kilichobeba ajenda nzito mno.
Wakati wakiendelea na mazungumzo mara kuna ujumbe mfupi wa maandishi uliingia kwenye simu ya Dkt Isaack Gondwe, akaufungua haraka na kuusoma.

,,,,,Yule binti Annah hajafa bado yuko hai, Inspekta Aron kamchukua kaondoka naye kwa siri hatujui alikompeleka, nitakupa taarifa zaidi naendelea kufuatilia,,,,,,,

Dkt Isaack Gondwe alikurupuka kutoka kwenye kiti akasimama ghafula kiasi cha kuwafanya watu waliokuwepo ndani ya chumba hicho wamtazame kwa pamoja.
“Aah! excuse me” (kumradhi) alisema Dkt Gondwe, akapiga hatua na kutoka nje ya kile chumba haraka.
Dokta Gondwe aliingiza mkono kwenye mfuko wa suruali akatoa simu yake ndogo Samsung, akaibonyeza haraka haraka akapiga namba aliyokuwa ameihifadhi kwa jina la ‘SELE GEREZA’ simu iliita kwa sekunde kadhaa mwisho ikapokelewa upande wa pili.

“Naam Mheshimiwa Waziri” Mkuu wa gereza la Kanondo SP Seleman alizungumza upande wa pili wa simu
“Tafadhali naomba kuongea na Osward sasa hivi kuna dharula”
“Mheshimiwa kwa sasa wafungwa wapo kantini wanakula, subiri kama dakika 15 hivi”
“Afande Sele hivi unaelewa mtu akisema ni dharula, kwanza Osward sio mfungwa yupo hapo kusubiri tarehe ya kesi yake kusikilizwa”
“Anatuhuma za mauaji ndio sababu yuko hapa, najua unaelewa taratibu zetu Mheshimiwa Waziri sipendi tubishane subiri kidogo nijaribu kukusaidia”
“Sawa nasubiri”
Simu ikakatwa, Dokta Gondwe akabaki amesimama nje ya kile chumba ambacho ndani yake kulikuwa na kikao cha siri kikiendelea. Habari za Annah kuwa hai zilimchanganya sana mbaya zaidi wakati wanafanya mauaji yeye na Tino hawakuwa wamefunika sura zao hivyo ilikuwa ni hatari kubwa kama Annah atanusurika kifo.
“Doctor, there’s something wrong?”(Daktari kunakitu hakipo sawa) Dokta Gondwe alishtushwa na sauti ya mzungu mmoja aliyetoka nje kumtazama.
“Nothing wrong Mr Codrado, two minutes please am coming”(Hakuna shida bwana Codrado, dakika mbili tafadhali nakuja)
“It’s you’re time to talk Doctor Gondwe, let’s go inside please we don’t have time”(ni zamu yako kuongea Dokta Gondwe, tuingie ndani tafadhali hatuna muda) alisisitiza yule mzungu na mara hiyo simu ya Dokta Gondwe ikaita.
“Dakika moja nakuja”
“What?”(nini?)
“Moja tu moja bwana Codrado”
“What do you mean!?”(unamaanisha nini!?) aliuliza Codrado akiwa hajaelewa kiswahili
“One minute”(dakika moja) Alisema Dkt Gondwe, Codrado akarudi ndani akionekana kutofurahishwa na alichokifanya Waziri wa afya. Punde tu baada ya Codrado kuondoka dkt Gondwe akapokea simu haraka
“Baba mkwee” sauti nzito ya kiume ilisikika upande wa pili wa simu ile
“Ndiyo Osward ni mimi, tafadhali sogea sehemu salama tuzungumze jambo”
“Nimeshasogea baba hivi ni kweli mmeshindwa kufanya chochote hadi sasa nakalibia kumaliza miezi miwili huku gerezani” Osward alilalamika
“Usijali mwanangu tupo kwenye hatua za mwisho mashahidi wote tumesha wamaliza nakuhakikishia safari hii tukirudi tena mahakamani unaachiwa huru”
“Asante mkwe nikitoka tu cha kwanza nafunga ndoa na binti yako Najma”
“Sawa lakini hilo tutaongea ukitoka, kuna kitu nataka kukuliza”
“Uliza tu baba mkwe”
“Hivi wakati unafanya mauaji yule binti wa yule mzee naye alikuona?” Aliuliza dkt Gondwe akiwa na shauku ya kusikia jibu kutoka kwa Osward.
“Kale kabinti wanakaita mmm! Annah si ndiyo?”
“Ndiyo Annah huyo huyo”
Osward alibaki kimya kwa muda akijalibu kuvuta kumbukumbu siku aliyofanya mauaji.
“Kwa kweli kumbukumbu zangu hazipo sawa baba mkwe, sikumbuki kitu kuhusu Annah”
“Dah! hii ni kazi nyingine sasa”
“Kivipi mzee?”
“Tulifanikiwa kuwakamata familia nzima tukawapiga risasi wote lakini kwa bahati mbaya Annah hajafa yupo kwenye mikono ya Inspekta Aron sasa hivi”
“Aron yule mdogo wake na Tino”
“Ndiyo, jamaa anatusumbua sana yule”
“Sasa sikia baba mkwe, uweni wote, muueni huyo binti haijarishi aliniona au hakuniona muueni na huyo Inspekta Aron hapo mtakuwa mmemaliza kila kitu” Osward aliongea kwa msisitizo.

“Sawa tutafanya hivyo lakini kuhusu kumuua Inspekta Aron hilo tusubiri kwanza, baadae Osward nipo kwenye kikao muhimu nitakupigia tena” Alisema Dkt Gondwe kisha akakata simu.

Osward alibaki amesimama wima akionekana kutofurahishwa na kauli ya mwisho kutoka kwa mheshimiwa Waziri wa afya. Osward alimchukia sana Inspekta Aron huyu ndiye alikuwa chanzo cha yeye kufunguliwa tuhuma za mauaji na alikuwa akipambana kwa nguvu zote kukusanya ushahidi kuhakikisha Osward anafungwa. Osward aliamini kama Inspekta Aron atakufa basi kila kitu kitakuwa rahisi kwake.

“Wanamlealea kwa sababu ni mdogo wake na Tino si ndiyo, basi mimi siwezi kuendelea kuvumilia” Osward aliongea kwa jazba huku akibinyabinya simu ya mkuu wa gereza, akapiga namba fulani na kuweka simu sikuoni, iliita kwa muda mwisho ikapokelewa.

“Oya big! Osward hapa naongea, nakuhitaji hapa magereza chapu kwa haraka” Osward aliongea kwa kifupi kisha akakata simu, alitembea taratibu hadi pale alipomuacha mkuu wa gereza SP Seleman akamrudishia simu yake.

“Vipi rudi sasa kwa wenzako mbona umekaa tena, mfuata askari yule pale anakusubiri akusindikize” alisema SP Seleman baada ya kuona Osward anakaa badala ya kurudi kwa wafungwa wenzake.
“Kun mtu nimemwita nina mazungumzo naye muhimu”
“Sikiliza Osward, najua wewe ni mtu mkubwa unawatu huko nje baba yako mzee Matula ni tajiri mkubwa pia Waziri wa afya anakukingia kifua lakini nataka kukwambia ukiwa hapa jaribu kuwa na nidhamu, wewe hauna tofauti yoyote na wenzako waliopo humu ni lazima ufuate kanuni na taratibu zetu, kukupa simu yangu ni heshima tu kwa mheshimiwa Waziri na si vinginevyo, tabia zako tangu umeingia hapa zimekuwa ni mbovu na hazivumiliki tena naongea kama mkuu wa gereza” SP Seleman alifoka akimtazama Osward kwa macho makali. Osward hakujibu chochote, alimtazama tu SP Seleman namna alivyokuwa akifoka, akatabasamu.
“Wapi nitakutana na mgeni wangu?” Osward aliuliza akionyesha wazi kuwa maneno ya Seleman hayajamuingia hata kidogo.
SP Seleman alitoa ishara fulani kwa askari aliyekuwa karibu, askari akasogea na kumtaka Osward amfuate. Wakaongozana hadi eneo maalumu ambalo wafungwa hukutana na watu wengine kutoka nje ya gereza kama vile ndugu na jamaa zao wanaokuja kuwatembelea.
Osward alimkuta mtu aliyewasiliana naye kwenye simu dakika chache zilizopita tayari ameshafika amekaa anamsubiri. Alikuwa ni mwanume mnene, mrefu mweusi karibu kila mahali isipokuwa viganja vya mikono yake pekee. Mwili wake ulikuwa umejazia na endapo ukimuona hauna sababu ya kujiuliza mara mbili mbili kuwa huyu ni mtu wa mazoezi tena sio mazoezi tu bali mazoezi makali.

“Ooh Big’ umeshafika tayari”
“Yeah, unanijua mimi mambo yangu nayaendesha kizungu”
“Hahahah kama kawaida yako”
“Vipi unatoka lini humu? kambini mambo hayaendi bila wewe mkuu” aliuliza yule bwana wa miraba minne
“Soon nitaungana na ninyi, sasa sikia kuna kazi ndogo hapa nataka nikupe”
“Ipi hiyo nambie”
“Unamjua yule askari jau ambaye ni chanzo cha mimi kuwa huku”
“Ee si yule mdogo wake Tino, anaitwa Aron”
“Yes! huyo huyo”
“Vipi tumuondoe?”
“Hayo ndio majibu, bila hivyo nitaozea humu ndani, yule jamaa jau sana wanamlealea kwa sababu ni mdogo wake Tino”
“Haina noma Osward ni hilo tu au kunalingine?”
“Ni hilo tu ila hakikisha kifo chake kisilete utata si unamjua kaka yake naye ni balaa jingine sitaki mambo mengi mimi” Osward alisisitiza

Je nini kitafuata?
Aron atakuwa salama?
Na je atafanikiwa kumlinda Annah?
Vipi kuhusu kile kikao cha Waziri wa afya na wazungu kutoka Mexico?

Acha comment, kupata mwendelezo