Simulizi: Mpenzi wangu Amina.(01)

Mwandishi: Salum Kalase

Sehemu ya kwanza.

Maisha ni kuchagua na mimi nilichagua kumpenda Amina katika maisha yangu yote bila kujali ni nini kitakachotokea katikati yetu.

Ngoja kwanza, kwa majina naitwa Gift Mathayo Lugwisha ni mtoto wa pekee nyumbani kwetu, baba huwa anadai hakutaka iwe hivyo lakini ndio ishakuwa hivyo, ndoto yake ilikuwa ni kuwa na watoto kumi na mbili yaani alipanga kumiliki timu nzima na kocha wake lakini haikuwa hivyo kwani mama alimsaliti baba, hivyo baba akaamua kumpatia talaka yake mama na akanichukua mimi kwenda kuishi nae. Sijawahi kumwona tena mama yangu hadi leo.

Baba naye hakutaka tena kujiingiza kwenye ndoa , hivyo alinilea peke yake kwa msaada mkubwa wa bibi yaani mama yake baba.

Kiukweli nilipatiwa malezi bora sana anayopaswa kupatiwa mtoto hadi nafikia umri wa kujitegemea sikumbuki kujihisi mpweke kabisa kila nilipokuwa nyumbani.

Naposema nyumbani namaanisha nyumbani tu, yaani nyumbani kwa baba na bibi yangu ila tofauti na hapo maisha yangu yamekua na upweke mkubwa sana na hiyo ni kwa sababu ya machaguzi yangu.
Kama nilivyosema mwanzo maisha ni kuchagua, na mimi niliamua kuchagua maisha ya upweke kwa sababu ya kumpenda mwanamke mmoja tu naye si mwingine bali ni Amina, Kivipi?

Mimi na Amina tulikutana mara ya kwanza mwaka 2014 wakati naingia kidato cha nne katika shule moja inayopatikana huko Mwadui Shinyanga ya kuitwa Mwadui Secondary School. Mimi nilikua muhamiaji katika shule ile vivyo hivyo kwa Amina naye alikuwa muhamiaji pale.

Kwa kuwa wote tulikua wahamiaji haikutuwia ugumu kufahamiana kwani nakumbuka mimi ndio nilitangulia kufika shuleni, na baada ya wiki moja Amina naye akafatia, Siwezi kuisahau siku ya kwanza namuona Amina, naikumbuka vizuri sana siku ile hadi hii leo, ilikuwa ni kwenye kipindi cha Mathematics, kipindi changu pendwa sana lakini cha ajabu siku hiyo nilikua najihisi usingizi balaa, hivyo sikuwa namsikiliza kabisa mwalimu kwani usingizi ulikua umenizidia na nilikua nalala kila nilipokua napata muda japo kwa kuiba ili nisionekane na mwalimu.

Ndipo mlango wa darasa letu ukafunguliwa, macho ya wanafunzi wote darasani yakatazama mlangoni kuona ni nani anayeingia Kasoro mimi ambae nilikua bado nipo bize na usingizi wangu.

Akaingia mwalimu wa nidhamu Mr Justus akiwa anaongozana na Amina kisha akasalimiana na mwalimu mwenzake na kumweleza ametuletea mwanafunzi mpya ambae alimuamuru ajitambulishe “Hi!!! My name is Amina Rashid(Habari zenu, Majina yangu naitwa Amina Rashid)” Amina alijitambulisha kwa sauti moja nyororo ambayo sikuwahi kuisikia kutoka kwa mtu yeyote yule tangu dunia hii iumbwe, sauti ile ilinifanya niamke kutoka usingizini na kutazama mbele, La haula!!! Haikuwa sauti tu, hata urembo aliokuwa nao Amina nikiri kusema kuwa hakuna mwanafunzi wa kiume mle darasani ambae hakummezea mate.

“Gift hiyo siti pembeni yako anakaa nani?” Mwalimu aliniuliza
“Haina mtu mwalimu” Nilimjibu haraka haraka mwalimu ambae alimwelekeza Amina aje kuketi kwenye siti ya pembeni na ninapokaa.

Ni kama Mungu alikua upande wangu, kwani niliona kama kila kitu kinatokea kwa haraka sana “Mambo” Amina alinisalimia huku akiwa anatabasamu, tabasamu lile likanifanya niione sifa nyingine ya Amina kwenye uso wake, Amina alikua na vishimo viwili kwenye mashavu yake yaani dimpozi, ugonjwa wangu mimi huo, kiukweli niliweweseka nikashindwa hata kuijibu ile salamu, nikabaki namtazama tu nisiongee kitu.

Washikaji zangu walikuwa wananichora (wananitazama) wakaanza kucheka chini chini kwa kuniona domo zege. Amina hakujali sana mimi kutokumuitikia salamu yake, akavuta kiti chake na kuketi ili amsikilize mwalimu aliyokuwa anayafundisha.

Kipindi hakikupanda tena, akili yangu yote ilikuwa kwa Amina , muda mwingi niliutumia kumtazama tu, sikuwa na nguvu za kuacha kuitazama sura yake iliyokuwa imejua kupangiliwa na mwenyeji Mungu.
“Unanitazama sana shida nini?” Huo ulikuwa ni ujumbe wa kikaratasi ambacho Amina aliamua kuniandikia baada ya kuona namtazama sana. Ujumbe ule ulinifanya niache kumtazama na kuangalia mbele bila kumjibu chochote kile.

“Mbona haujanijibu, nimekuuliza shida nini” Amina alinipatia kiujumbe kingine tena, nikakisoma, na nikaamua kukijibu
“Nikisema wewe ni mrembo sana utaniamini?” Amina alisoma ujumbe wangu wa karatasi, nikamwona anatabasamu lakini hakunijibu chochote kile zaidi ya kukikunja kile kikaratasi na kukiweka kwenye begi lake.
“Nimekwambia wewe ni mrembo sana” Nilimtumia meseji nyingine Amina ambayo nayo aliisoma na kuiweka kwenye begi lake

Kitendo kile kikanitia unyonge sana, nikajihisi nimewahi sana kuzicheza karata zangu “Dah itakuwa ameshaniona muhuni” nilijiwazia na tayari nilijipatia majibu kuwa ndio hivyo nishampoteza Amina wangu kizembe namna hiyo.

Kipindi cha Mathematics kiliisha, vikafatia Vipindi vingine ambavyo navyo vilianza na kuisha bila ya mimi na Amina kusemezana. Wakati tupo kipindi cha mwisho kabisa cha siku hiyo zikiwa zimebaki kama dakika ishirini hivi kipindi kuisha, nikawaza kama kumpoteza Amina nishampoteza sasa kwanini nisimpoteze mazima kwa kujilipua kabisa na kuzielezea hisia zangu kwake ndipo nikaamua kuchukua karatasi na kumwandikia maneno haya,

“Mbona hivyo Amina unanitisha ujue” kisha nikampatia asome huku mimi nikiwa nimetazama mbele.
Haikuchukua dakika Amina akanigusa na kunipatia kikaratasi alichokuwa amenijibu “Kwanini unasema hivyo?”
“Kosa langu nini sasa hapa kukusifia au, mbona umeninunia ghafla”
“Hapana hata sijakununia mbona”
“Sasa kama haujaninunia mbona hukunijibu sms yangu nilivyokwambia wewe ni mrembo?”
“Naomba basi tuzungumze kipindi kikiisha wanafunzi wenzetu wakishaondoka darasani sawa” Maneno ya Amina yalinishtua kidogo moyo wangu, sikutegemea kama angeweza kuniambia vile, yaani atake kuzungumza na mimi baada ya vipindi kuisha, tena peke yetu mimi na yeye tu.
“Sawa” Nilimkubalia.

Kipindi cha mwisho kiliisha, wanafunzi wakaanza kuondoka kurudi mabwenini kwa lengo la kwenda kujiandaa na chakula cha mchana. Mimi na Amina hatukuondoka, tulibaki tumeketi kwenye siti zetu tukiwa kimya bila kuongea chochote kile. Sijui Amina alikua anawaza nini muda ule lakini kwa upande wangu sikuwa najua cha kuongea baada ya wanafunzi wote kuisha mle darasani.
“Vipi unanitaka?”

“U….u…Unasema?” Nilijikuta nauliza swali baada ya kujibu swali aliloniuliza Amina.
“Nimekuuliza kama unataka kuwa na mimi kwenye mahusiano? Amina aliniuliza tena swali lake na mara hiyo alikuwa amelifafania zaidi ili nimwelewe alichokuwa ameniuliza. Nilimtazama kwa muda kabla ya kumjibu, Amina alikua amenikazia macho, hakuwa na aibu hata kidogo Tofauti na mimi niliyekuwa naona aibu hata kumtazama,
“Nimekuuliza swali mbona haunijibu” Amina alinisemesha tena
“Swali lako gumu sana ujue”
“Kwahiyo haujui unachotaka kutoka kwangu si ndio?”
“Hapana sio hivyo Amina”
“Ila kumbe nini sasa…….”
“Nikisema kwamba sitaki kuwa na wewe nitakuwa nakudanganya nahitaji sana kuwa na wewe lakini……….” Kabla hata sijamalizia kuongea Amina alinikatiza

“Sawa tutakua wapenzi kuanzia leo sitaki kujua hizo sababu nyingine” Amina aliniambia vile huku akitabasamu. Nadhani udhaifu wangu mkubwa kwa Amina ni tabasamu lake naweza kusema hivyo kwani nazikumbuka vyema hisia zangu muda ule Amina ananiambia kuwa tumeshakuwa wapenzi, ukweli ni kwamba sikuwa tayari bado kuwa na Amina kimapenzi lakini lile tabasamu lake ndilo lililoninyima ujasiri wa kumkatalia alichokuwa amenieleza.

Sijui hata kwanini nilitaka kukataa kuwa naye kwani Amina alikuwa na kila sifa za mwanamke ambazo mwanaume rijali alizihitaji kutoka kwa mwanamke wake.
“Tutakutana jioni sasa mpenzi wangu” Amina alinieleza vile kisha akachukua begi lake na kuondoka zake kwenda bwenini kwao, aliniacha nikiwa bado nimesimama pale kwenye siti yangu nikiwa siamini kilichokuwa kimetokea.

Acha Comment ili Upate mwendelezo